Kampuni ya mawasiliano ya simu ya Vodacom Tanzania imesema imefurahishwa sana na namna ambavyo washiriki wa Dance100 wamekuwa na ubunifu wa hali ya juu na kufanya fainali za Dance100 kuwa za aina yake mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kutoka Vodacom Jacquiline Materu amesema Dance100 inazidi kuimarika siku hadi siku na ubunifu ambao unaoneshwa na washiriki hao kuanzia mavazi na zana walizotumia umedhihirisha kwamba katika jamii kuna vipaji vingi sana ambavyo vinahitaji kuvumbuliwa.

Materu ameongeza kuwa Vodacom inaendelea kudhamini shughuli mbalimbali zinazohusu vijana hapa nchini ikiwa ni pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kutambua mchango wa kundi la vijana ndani ya jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Umma wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu amepongeza hatua ya majaji wa Dance100 kuwatembelea washiriki wa Dance100 katika maeneo yao ya mazoezi na kuwafundisha mbinu za namna ya kuweza kuwa wachezaji wazuri.

Shindano la Dance100 limefikia tamati kwa kundi la ‘Team Makorokocho’ wameibuka mabingwa ambapo wamejinyakulia kitita cha shilingi milioni 7, Mshindi wa pili kundi la J Combat kutoka Zanzibar wamejinyakulia shilingi milioni 2 huku kundi la tatu D.D.I Crew limejinyakulia shilingi milioni 1.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *