Taasisi ya utafiti wa magonjwa ya binadamu, NIMR imethibitisha kugunduliwa kwa virusi vya Zika nchini Tanzania.

Mkurugenzi wa NIMR, Dkt Mwele Malecela amesema kuwa virusi hivyo vimepatikana mkoani Morogoro, na Mkoani Geita.

Utafiti huo ulifanyika kutokana na uhalisia kuwa kuna mazingira yanayowezesha kuzaliana kwa mbu wanaoeneza virusi hivyo.

Dkt Mwele Malecela amesema kwamba kwa sasa serikali inaangazia kuzuia wajawazito wasiumwe na mbu ambao wanaaminika kueneza virusi hivyo.

Virusi vya Zika zimekuwa vikisababisha watoto kuzaliwa wakiwa na ubongo uliodumaa na vichwa vidogo katika mataifa ya Amerika Kusini haswa nchini Brazil.

Mapema mwaka huu, serikali ya Tanzania iliwaagiza madaktari wote kuwa macho kuhusu hatari ya virusi hivyo mlipuko ulipotokea nchini Brazil.

Virusi vya Zika huenezwa sana na mbu ingawa kumeripotiwa pia visa vya watu kuambukizwa virusi hivyo kupitia kufanya mapenzi.

Haijabainika iwapo aina ya virusi vya Zika vilivyopatikana Tanzania ni vile ambavyo vimekuwa vikisababisha watoto kuzaliwa na vichwa vidogo Amerika Kusini.

Virusi vya aina hiyo viligunduliwa kwa mara ya kwanza barani Afrika katika visiwa vya Cape Verde mwezi Mei mwaka huu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *