Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa ametakiwa na viongozi wa vyama vya siasa nchini Burundi kutokuwa mzungumzaji bali awe msikilizaji tu kwenye kikao cha usuluhishi kitakachofanyika jijini Arusha.

Viongozi hao wameyasema hayo jana jijini Arusha wakati wakitoa maoni wakati wa kikao cha siku moja kwa ajili ya kujadili hatma ya amani nchini Burundi.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo, Bigirimana Jacquees amesema hawapingani na msuluhishi wa mgogoro huo ambaye ni Rais Mkapa, bali wanachotaka ni kutokuwa mzungumzaji zaidi katika kikao hicho.

Amesema wao wanataka wazungumze wenyewe kwa wenyewe kwa kutumia lugha zao na kunyoosheana vidole, badala ya msuluhishi huyo kuwa mzungumzaji zaidi.

Awali mmoja kati ya mawakili wa kujitegemea kutoka Burundi, Ali Mbongo amesema Warundi wanahitaji amani ikiwemo Kiswahili kupewa kipaumbele kwani pia katika nchi hiyo kuna kabila la Waswahili ingawa halipewi nafasi yoyote kwa ngazi za jamii.

Amesema Waswahili hao walifika Burundi zamani, lakini cha ajabu hawapewi nafasi yoyote ya uongozi wala kusikilizwa, lakini ni raia wa Burundi na wanapata taabu kutokana na kutotambuliwa kisheria.

Rais Mkapa aliongoza kikao kilichofanyika mwaka jana Burundi kwa kupeleka maazimio yao kwa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), lakini kuna mambo aliyasema ambayo hawajapendezewa nayo ingawa hakuwa tayari kuyataja, ila alisisitiza ni muhimu wao kama makundi ya vyama vyake vya siasa kusikilizwa wenyewe kwa wenyewe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *