Vikao vya Kamati za kudumu za Bunge vinatarajiwa kuanza Jumatatu wiki ijayo mjini Dodoma, vitapokea maoni ya miswada mbalimbali ikiwemo Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 na taarifa za utendaji wa wizara mbalimbali.

Vikao hivyo vitakavyomalizika Oktoba 30, mwaka huu pia vitapokea uchambuzi wa taarifa kuhusu hesabu zilizokaguliwa.

Vikao hivyo ni maandalizi ya Mkutano wa Tano wa Bunge utakaoanza Novemba Mosi, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi na Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Ofisi ya Bunge, Dodoma, ilieleza kuwa “Kamati ya Katiba na Sheria itajadili muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 3 wa mwaka 2016 na itakuwa na vikao vya kupokea maoni ya wadau kuhusu muswada huo Oktoba 21.

Sheria hiyo ina jumla ya sheria tisa zitakazofanyiwa marekebisho na muswada huu”. Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii itajadili muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa mwaka 2016 na itapokea maoni ya wadau Oktoba 19.

Mbali na kamati hizo za kisekta, pia Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo itafanya mikutano ya kupokea maoni ya wadau Oktoba 18 na 27 kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa na serikali katika Mkutano wa Nne wa Bunge.

Pia Kamati tisa za kisekta zitapokea taarifa ya utendaji wa wizara zinazosimamiwa na kamati hizo ikiwemo Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama itakayopokea na kujadili taarifa za wawakilishi wa Bunge katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika katika Jukwaa la Bunge (SADC-PF), ACP-EU (Umoja wa nchi za Afrika, Caribean na Pasific pamoja na Umoja wa Ulaya-EU) na CPA (Bunge la Jumuiya ya Madola).

Kamati nyingine zitakazohusika na kupokea taarifa za utendaji za wizara ni Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) ambayo itapokea na kujadili taarifa ya Uwekezaji unaofanywa na mashirika na taasisi ya umma tisa na Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa itafanya ziara mbili mkoani Dodoma kufuatilia utendaji wa wizara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *