Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT),  umefanya mabadiliko ya makatibu wa wilaya, ambapo baadhi ya watumishi wake ambao ni madiwani wa viti maalumu wamejikuta wakipelekwa nje ya halmashauri zao.

Mabadiliko hayo yamekuja ikiwa ni mwezi mmoja baada ya CCM kupitisha mabadiliko ya katiba yake katika Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika Machi 12, mwaka huu, mkoani Dodoma.

Mabadiliko hayo yameeleza wazi kuwa hivi sasa mtu mmoja cheo kimoja, tofauti na zamani ambapo baadhi ya viongozi ndani na nje ya chama hicho walikua wanajilimbikizia vyeo.

Uhamisho huo umetajwa kuwavuruga baadhi ya makatibu ambao pia ni madiwani wa viti maalumu katika halmashauri zao wanazotumikia.

Baadhi ya makatibu waliohamishwa na maeneo wanayokwenda kwenye mabano ni Huba Issa anayetoka Kinondoni kwenda Newala), Monica Nyagu (Kongwa – Manyoni), Joan Mazanda (Dodoma Mjini – Singida Vijijini), Mwashamba Shekue (Tanga Jiji – Kilindi) na Hilda Mdaki (Gairo – Rombo).

Katibu wa UWT Taifa, Amina Makilagi alisema mabadiliko hayo hayawazuii madiwani hao kutekeleza majukumu yao.

Amesema tangu mwaka 1995 baadhi ya makatibu walikuwa ni madiwani lakini hilo halikuathiri udiwani wao bali ni namna tu ya kujipanga.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *