Mwandishi wa vitabu mashuhuri nchini, Eric Shigongo ameendelea kutoa ushauri wa kimaisha kwa mwanamuziki wa Bongo Fleva nchini Alikiba pamoja na uongozi wake chini ya Seven Mosha.
Shigongo ambaye ni mmiliki wa mmiliki wa kampuni ya Global Publishers ameamua kutoa ushauri kwa Alikiba baada ya kutoa ushauri kama huo kwa Diamond wiki iliyopita mpaka kusababisha bifu kati yake na meneja wa Diamond, Babu Tale.
Shigongo kupitia akaunti yake ya Instagrama ameandika ushuri kama ifuatavyo
Kama nilivyosema kwa Diamond kwenye ushauri wangu kwamba alifikishwa hapo alipo na mashabiki zake, anatakiwa kuwaheshimu sana hata kama ni wachache au wengi kwani pasipo kufanya hivyo, mambo yanaweza kumuharibikia kama tulivyoona kwa wanamuziki wengi waliopita.
Bado nitaendelea kusema hata kama kuna watu watatokea kunitukana, sitojali kwa kuwa kile ninachokiongea, nina uzoefu nacho kwa miaka ishirini niliyokuwa katika tasnia ya uandishi wa habari.
Gharama za shoo za Ali Kiba ni za juu sana kiasi kwamba hata wale mashabiki wengine wadogo wamekuwa wakishindwa kuhudhuria kwa kuwa mapromota wanaoandaa huweka kiingilio kikubwa ili kupata faida na hivyo wale mashabiki wanaomuhusudu hasa wa huku kwetu uswahilini kushindwa kutazama shoo zake live.
Kuna mambo machache ambayo Ali anatakiwa kufanya ili aendelee kuwa juu zaidi na zaidi, kama anasoma, naomba ayasome haya. Mambo yenyewe ni haya hapa
- ‘Detachment from fans’, hii ina maana ya kujitenga kutoka kwa mashabiki zake. Linaweza kuonekana kuwa jambo dogo lakini limekuwa likiwaangusha wanamuziki wengi duniani. Hili ni la kwanza ambalo anatakiwa kujiepusha nalo kama atataka kuwa juu kwa kipindi kirefu.
- Ali ni mnyenyekevu, hataki makuu lakini kwa kazi yake ilivyo inambidi kidogo aongeze thamani, hapa nina maana kwamba Ali ajiepushe na suala la kusafiri bila meneja anapokuwa ndani au nje ya nchi kwenye shoo. Simaanishi kwamba hasafiri naye, hapana, namaanisha kwamba asifikirie kutokusafiri naye kwani hii huongeza thamani ya msanii anapoongozana na timu yake, hasa meneja au mameneja.
- Asiyumbishwe na ushindani. Huu upo kote duniani na ndiyo maana ni rahisi kusikia Nicki Minaj anashindana na Iggy Azalea. Anachotakiwa ni kuweka chapa zake katika aina fulani ya muziki ili vizazi vijavyo viweze kumkumbuka kwa muziki wake fulani kama anavyojulikana Michael Jackson kwa muziki wa Pop.
- Afanye sana kazi za kijamii. Hili linaonekana kuwa jambo dogo sana lakini unapoamua kufanya kazi za kijamii inakuweka karibu na mashabiki zako na pia unabarikiwa kulingana na kile unachokifanya.
- Asiweke nguvu zake nyingi katika mambo yasiyokuwa na tija. Hili huwa linamfanya mwanamuziki kupotea haraka. Skendo hazikufanyi kusikika bali zinakufanya kupotea kwani mashabiki zako watakuwa wanahitaji muziki, hawahusikii inavyotakiwa, skendo zinakuwa nyingi kuliko kazi. Kiba amejulikana kwa sababu ya muziki, hajajulikana kwa sababu ya skendo, waliosikika kwa skendo acha wafanye skendo ila kama umejulikana kupitia muziki, fanya muziki.
- Awasaidie wazazi wake kwa kila kitu. Wazazi ndiyo nguzo muhimu sana hapa duniani. Unaweza kuona unafanikiwa lakini unapomwacha mzazi ni lazima kutakuwa na vitu vibaya vitatokea, huwezi kuviona sasa hivi, kuna siku ukishaanza kushuka, kuna sauti moja ya upole itasikika moyoni mwako, itakwambia kwamba tatizo halikuwa kukosa thamani, halikuwa kukosa mapromota, tatizo kubwa lilikuwa ni mama au baba kwani Mungu aliwachagua hao wawe wazazi wako kwa makusudi yake.
- Nilipokutana na Seven na kuzungumza naye, nilibahatika kumwambia kuhusu gharama kubwa, kwa unyenyekevu mwingi, alikiri kuwepo kitu hicho na ndiyo maana shoo zake si nyingi sana nyumbani. Namnukuu Seven: “Ni kweli Eric, gharama zipo juu lakini ndivyo tunavyotoza hata huko nje. Ili kidogo tufanye shoo za kutosha hapa nyumbani, basi wadhamini wajitokeze wengi japo na sisi gharama zishuke kwa kuwa wakijitokeza wengi, na sisi tutaingiza kingi hivyo hata malipo yatakuwa madogo. Kama akija mdhamini mmoja, inajulikana kwamba lazima shoo iwe ya gharama sana. Lakini mbali na hilo Eric, naandaa kufanya shoo za hisani mara kwa mara ili kuisaidia jamii kwani naamini itamfanya Ali kuwa karibu na mashabiki zake.”
Aliendelea kuongea kwamba malipo ya nyumbani yana kila sababu ya kushushwa kwa kuwa Tanzania ipo chini kiuchumi, si kama Afrika Kusini au nchi za Ulaya. Mashabiki watuelewe tu kwamba tunajua kwamba wanatofautiana kifedha, hatuwezi kuwatenga kwa kuwa wote ni mashabiki zetu, tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha shoo zinamfikia kila mtu,” alimalizia Seven.