Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema kuuawa kwa balozi wa taifa lake nchini Uturuki Andrey Karlov siku ya jana ni uchokozi ambao lengo lake ni kuvuruga juhudi za kutafuta amani Syria.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amesema kuuawa kwa balozi huyo ni shambulio dhidi ya taifa la uturuki.

Karlov aliuawa kwa kupigwa risasi na afisa wa polisi ambaye hakuwa kwenye zamu, alipokuwa anatoa hotuba kwenye maonesho ya picha katika mji mkuu Ankara.

Picha za video zilimuonesha mshambuliaji huyo akiwa amevalia suti na tai akimfyatulia risasi balozi huyo kutoka nyuma akisema kwa sauti ujumbe kuhusu mji wa Aleppo.

Taarifa zinasema muuaji ni Mevlut Mert Aydinta mwenye umri wa miaka 22 ambaye alikuwa anahudumu katika kikosi cha polisi kupambana na fujo mjini Ankara.

Kisa hicho kilitokea siku moja baada ya maandamano kufanyika Uturuki kupinga hatua ya Urusi kumuunga mkono Rais wa Syria Bashar al-Assad.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *