Muungano wa upinzani nchini Kenya NASA umesema kuwa utamtangaza atakayeshikilia bendera yake ya urais mnamo tarehe 27 mwezi Aprili 2017.

Akizungumza katika mkutano wa kumlaki gavana wa kaunti ya Bomet Isack Ruto kujiunga na muungano huo kama mmoja wa viongozi wakuu wa chama hicho.

Waziri wa zamani wa maswala ya kigeni ambaye pia ni seneta wa kaunti ya Bungoma Moses Wetangula amesema kuwa kiongozi huyo atatajwa katika mkutano utakaofanyika uwanja wa Uhuru Park uliopo katikati ya jiji la Nairobi.

Amesema kwamba tayari viongozi hao ambao wamekuwa wakikutana kwa takriban siku tatu zilizopita wamepiga hatua ya kumchagua mmoja wao kuongoza muungano huo.

Viongozi wakuu wa muungano wa NASA ni aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga wa chama cha ODM, aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka, wa chama cha Wiper, Moses Wetangula wa chama cha Ford Kenya na Issack Ruto wa chama cha mashinani CCM.

Wetangula amesema kuwa kiongozi atakayetangazwa atakuwa amechaguliwa na viongozi wote watano na kwamba hakuna kiongozi atakayekuwa na pingamizi miongoni mwao.

Amesema kwamba wafuasi wa NASA watakaopinga tangazo hilo watachukuliwa kwamba wanaunga mkono chama tawala cha Jubilee.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *