Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa atabadilisha uongozi wa juu wa shirika la Posta nchini kutokana na kushindwa kuendeleza shirika hilo kwa kasi inayotakiwa.

Mbarawa amesema hayo jana alipofanya ziara katika ofisi za shirika hilo za Posta jijini Dar es Salaam na kujionea shughuli zikifanyika na baadaye kuzungumza na wafanyakazi Makao Makuu ya TPC.

“Unajua ifikie mahali tuambizane ukweli, tukianza kuogopana hapa kwamba kesho nakuletea hela, hakuna hela, hela mnayo mna maghorofa kwanini hamfanyi kazi, tumeenda asubuhi posta hapa , posta nzima ina wateja 20 ni aibu. Mnakaa mnafanya nini hamuendi kutangaza Posta, hamuhangaiki kutafuta wateja,” alisema Nbarawa.

“Ni lazima kufanya uamuzi. Inawezekana mzazi wako amefariki na amekuachia mali nyingi hivyo usipozitumia unakuwa masikini, shida yenu Posta ni uongozi. Hamjapata viongozi wa kusimamia Posta, sisemi hivyo kwa kuwa namwonea mtu bali ni hali halisi,” alisema Mbarawa.

Pia Mbarawa alisema, atamtafuta mtendaji mzuri na kumpeleka ili shirika liwe na mabadiliko kama alivyofanya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) na Shirika la Meli kwa kupeleka watendaji wenye maono ya mbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *