Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Florens Turuka amepiga marufuku uingizaji migomba na mazao yake kutoka Msumbiji kwa kuwa nchi hiyo imekumbwa na ugonjwa unaoshambulia zao hilo ambao kitaalamu unajulikana kwa jina la Panama Disease.

Dk Turuka alisema katika kuhakikisha mazao ya migomba hayaingii nchini kutoka Msumbiji, Tanzania imeweka wataalamu wake wa mimea katika mipaka na nchi hiyo, viwanja vya ndege na maeneo yote muhimu ili kuimarisha ukaguzi.

Amesema ugonjwa huo haujaingia nchini, lakini tayari wamechukua tahadhari kwa kuzuia uingizwaji wa mazao ya migomba kutoka Msumbiji kwa kuwa ugonjwa huo ni hatari.

Mbali na ugonjwa huo, pia Tanzania kwa sasa haiwezi kusafirisha matunda kwenda Afrika Kusini kutokana na kuwepo mdudu hatari wa matunda.

Dk Turuka amewaambia washiriki wa mkutano huo unaoshirikisha nchi 15 za SADC na COMESA kuwa mkutano huo ni muhimu katika kupanga mikakati ya pamoja kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mimea katika ukanda wa Afrika kwani magonjwa hayo katika sekta ya kilimo yanaathiri kwa kiasi kikubwa uzalishaji na uchumi wa nchi na wananchi wake na kusababisha kukosekana kwa uhakika wa usalama wa chakula na mazao.

Ugonjwa wa migomba huathiri uzalishaji kwa asilimia 70 katika nchi za SADC na husababisha hasara ya tani 1.52 za ndizi katika nchi hizo.

Pia alisema ugonjwa wa mahindi uliozikumba nchi za Afrika Mashariki ulitokea kuwa ugonjwa hatari na kuathiri zaidi uzalishaji wa mahindi na kutishia usalama wa chakula kwa kaya nyingi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *