Polisi wa Uingereza  wamesitisha kubadilishana taarifa za siri na Marekani zinazohusu shambulio la bomu la kujitoa muhanga mjini Manchester lililotokea siku ya Jumatatu.

Hatua  hiyo  ni kwasababu ya hofu ya kuvuja kwa  taarifa hizo katika vyombo vya habari nchini Marekani ambako kunaweza kuzuwia msako wa kumtafuta  mtu ambaye huenda  amehusika  katika  utengenezaji  wa  bomu ambaye hadi  sasa hajapatikana.

Iwapo itathibitishwa , hatua  hiyo  ya  kuzuwia  kupeana  taarifa  na mshirika  muhimu  kabisa  wa  Uingereza  katika  ulinzi na  usalama kutaonesha  kiwango cha  hasira  ya  Uingereza  kuhusiana  na kuvuja  katika  vyombo  vya  habari  nchini  Marekani  kuhusu  taarifa za  uchunguzi  wa  polisi.

Waziri  mkuu  wa  Uingereza  Theresa  May  atalizusha  suala  hilo wakati wa  mkutano wake  na  rais  wa  Marekani  Donald Trump leo, vyanzo  katika  serikali  vimelieleza  shirika  la  habari  la Reuters, baada  ya  gazeti  la  New York Times  kuchapisha  picha za  eneo  lililotokea  mashambulizi  mjini  Manchester  ambako watu 22 waliuwawa.

Picha  hizo  ni  pamoja  na  mabaki  ya  bomu  linaloshukiwa kutumiwa katika  shambulio  hilo, mfuko  wa  kubeba  mgongoni uliokuwa  umebebwa  na  mshambuliaji  wa  kujitoa  muhanga na kuonesha  damu  katika mabaki  ya  magari  yaliyoharibiwa.

Polisi  wa  Manchester wanamatumaini  ya  kurejesha  uhusiano  wa  kupashana  habari  za kijasusi  hivi  karibuni  lakini  kwa  sasa  imekasirishwa.

Baada  ya  shambulio  baya  kabisa  kuwahi kuwauwa  watu nchini Uingereza   tangu  mwaka  2005, polisi  imo  katika  msako kumtafuta  mshirika  ambae  inashuku  alimsaidia  Salman Abedi kutengeneza  bomu  hilo  lililowauwa  watu  22  siku  ya  Jumatatu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *