Shirikisho la soka barani Ulaya Uefa linatarajia kuwasilisha pendekezo kwa timu za bara hilo kupewa nafasi 16 kwenye mashindano ya kombe la dunia la mwaka 2026 ambapo timu zitakazoshiriki zitakuwa zimeongezwa na kufikia 48.

Shirikisho hilo la Ulaya pia litaomba Fifa kuzitenganisha timu za bara hilo wakati wa raundi ya kwanza ya kimakundi.

Awamu ya kwanza ya makundi 16 yanayoshirikisha timu 3 kila moja itafanyika kabla ya timu 32 kuendelea katika mchuano huo.

Rais wa Uefa Aleksander Ceferin amesema kuwa ombi hilo linawezekana na ni mpango wake kwa timu za bara hilo kufuzu katika raundi ya kwanza.

Ceferin alikuwa akizungumza katika mkutano wa kamati kuu ya Uefa mjini Nyon Switzerland.

Idadi ya timu zitaongezeka na kufikia 80 kutoka 64 lakini washindi bado watacheza mechi saba pekee.

Kinyang’anyiro hicho kitachukua siku 32 kukamilika hatua inayolenga kuzifurahisha klabu za Ulaya ambazo zilipinga mabadiliko hayo kutokana na mechi nyingi za kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *