Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Tanzania imebaki kuwa miongoni mwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara Barani Afrika, ambazo uchumi wake unakua kwa kasi.

Dk Mpango alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya uchumi wa taifa kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2016 na matarajio hadi Juni, 2017.

Alisema ukuaji wa uchumi ni mojawapo ya vitu vinavyotazamwa katika kutathmini afya ya uchumi wa taifa.

Akifafanua, alitoa mfano kwa baadhi ya nchi hizo kuwa mwaka jana Tanzania uchumi wake ulikuwa kwa asilimia 7.0 na mwaka huu unakua asilimia 7.2, Kenya mwaka jana ulikua asilimia 5.6 na mwaka huu unakua asilimia 6.0, Uganda mwaka jana ulikuwa asilimia 4.8 na mwaka huu unakuwa asilimia 4.9.

Kwa upande mwingine, amesema kuwa ustawi wa uchumi wa taifa unapimwa kwa kuangalia viashiria mbalimbali vikiwemo ukuaji wa pato la taifa, mfumko wa bei, thamani ya shilingi, mwenendo wa sekta ya kibenki na sekta ya nje na akiba ya fedha za kigeni.

Akizungumzia mfumuko wa bei, alisema ulipungua kutoka asilimia 6.5 Januari 2016 hadi asilimia 5.5 Juni 2016 na kupungua zaidi hadi asilimia 4.5 Septemba mwaka huu. Baadaye ulipanda kidogo mwezi Novemba na kufikia asilimia 4.8.

Amesema thamani ya shilingi ya Tanzania imeendelea kuimarika dhidi ya dola ya Marekani. Shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kati ya shilingi 2,167 hadi 2,199 kwa dola moja ya Marekani.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *