Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imesema, Oktoba 10, mwaka huu itatoa uamuzi wa maombi ya mke wa aliyekuwa bilionea jijini Arusha, marehemu Erasto Msuya, Miriam Msuya ya kufutiwa mashitaka ya mauaji ya wifi yake, Anneth Msuya.

Uamuzi huo ungetolewa jana lakini kesi iliahirishwa kwa kuwa, Hakimu Mkazi Magreth Bankika anayesikiliza kesi hiyo, hakuwepo mahakamani.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema, kesi ilitajwa kwa ajili ya kutolewa kwa uamuzi lakini hakimu anayeisikiliza hakuwepo hivyo uamuzi utatolewa Oktoba 10, mwaka huu.

Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Revocatus Muyela.

Muyela na Miriam wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji ya dada wa bilionea Msuya.

Washitakiwa kupitia kwa Wakili wao, Peter Kibatala wameiomba mahakama iwafutie mashitaka hayo kwa kuwa, hati ya mashitaka ina mapungufu na haioneshi kama walikuwa na nia ovu.

Amedai kuwa, washitakiwa wamekuwa wanateswa na kuwasababishia madhara mwili, hivyo kuomba mahakama iamuru uongozi wa jeshi la Magereza uwafanyie uchunguzi wa afya.

Inadaiwa kuwa, Mei 25, mwaka huu maeneo ya Kibada wilaya ya Kigamboni jijini Dar es Salaam, walimuua Anneth. Anneth aliuawa kwa kuchinjwa akiwa nyumbani kwake Kibada.

Wauaji hawakuchukua kitu chochote kwenye nyumba hiyo. Bilionea Msuya aliuawa Agosti, 2015 kwa kupigwa risasi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *