Hakuna anayepingwa ukweli kuwa dawa za kulevya ni janga kubwa sana kwa binadamu duniani. Uwezo mkubwa wa dawa hizo kudhoofisha mwili na akili ya mtumiaji hadi kumuondolea uwezo na ufanisi wa utendaji kazi pamoja na kumfanya tegemezi kwa dawa hizo umezifanya kupewa sifa kedekede na majina ya kila aina ili mradi kuashiria namna ambavyo zina athari kwa mtumiaji.

Sifa na majina haya hutegemea sana mtazamo wa mtumiaji, mtazamo wa mtu wa karibu na mwathirika, muuzaji na wanaharakati wanaopinga matumizi ya vilevi hivi ikiwa ni pamoja na taasisi za kiusalama ikiwemo Polisi.

Hivi karibuni sanaa ya Tanzania ilishuhudia mambo ambayo huenda miaka 30 iliyopita haikuwa ikiyatarajia kutokea kwenye sanaa ya muziki wa Tanzania.

Ukuaji mkubwa wa sanaa ya Tanzania unaojumuisha kuibuka kwa vipaji vingi zaidi, wasanii kulipwa fedha nyingi zaidi kwa kazi zao, wazalishaji muziki na wasimamizi kuongezeka na hata athari ya ushawishi wa tasnia hiyo kwa watu wa kawaidaikiwemo kuiga aina za kunyoa, uvaaji wa nguo n.k ni sehemu ya uthibitisho kuwa sanaa ya muziki hususani Bongo Fleva imepata mafanikio nchini Tanzania.

Lakini kama ilivyo ada, mafanikio huambatana na changamoto nyingi sana, na moja ya changamoto kubwa zilizojitokeza kwenye muziki wa Tanzania ni kuibuka kwa kasi kwa matumizi ya dawa za kulevya miongoni mwa wasanii wa muziki huo.

Kuna mifano mingi ya dhahiri ya wasanii ambao walikuwa wanatumia dawa hizo za kulevya (hususani baada ya kupata mafanikio kutokana na muziki) na wengine imewalazimu mpaka kuwekwa kwenye viruo maalum kwaajili ya kuwasaidia kuachana na matumizi ya dawa hizo.

Jambo linaloshangaza na kuvutia wengi ni ukweli kuwa watumiaji wengi wa dawa za kulevya daima huwa wanakanusha na kupinga vikali tuhuma hizo lakini mambo yabapowafikia pabaya hurejea kwa jamii ili iwasaidie.

Katika kukanusha huko wasanii hutuhumu watu kuwaonea wivu na kuwafuatilia maisha yao binafsi kitu ambacho ni haki yao kukifurahia (haki ya faragha – right to privacy).

Waswahili husema ‘lisemwalo lipo’ na kama hiyo haitoshi humalizia ‘kama halipo basi laja’ hii ni kudhihirisha kuwa kile mtu anachotuhumiwa nacho na yeye kukikanusha ni kitu cha kweli na kama bado hakijafanyika au kutokea basi ipo siku kitatokea kutokana na mwenendo wanaokuwa wanauona.

Je, wanaotoa habari kuhusu mienendo mibovu ya wasanii wetu hususani matumizi ya dawa za kulevya ni watu wabaya? Watengwe? Tumsubiri Young Dee mwingine aje atuambie kuwa yeye ‘ALIKUWA ANATUMIA’? au tujifunze kupitia kwa mastaa kama Ray C na Chidi Benz ambao waliendana na methali ‘Mficha maradhi, mauti humuumbua’?

Je, tutiliane shaka ili tuweze kusaidiana? AU ‘Tuelimishane kwa maneno matupu huku vitendo vikienda kinyume na maneno yetu’?

Je, tumsubiri Nyandu Tozi mwingine aje atuambie kuwa ‘HAKUWA ANAFAHAMU’ mshkaji wake wa karibu (Young Dee) alikuwa akitumia dawa za kulevya?

Tanzania WAKE UP!! Bongo Fleva WAKE UP!! Mastaa WAKE UP!!

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *