Mgombea urais wa chama cha Republican, Donald Trump amesema mpango wa mpinzani wake Hillary Clinton kuhusu kutatua mzozo Syria utaanzisha vita kuu ya tatu ya Dunia.

Trump amesema Marekani inafaa kuangazia zaidi kushinda vita dhidi ya kundi la Islamic State badala ya kulenga kumshawishi au kumshinikiza Rais wa Syria Bashar al-Assad kung’atuka.

Clinton amekuwa akipendekeza kutolewe katazo la ndege kutopaa katika anga ya Syria, mpango ambao baadhi wamesema huenda ukasababisha mgogoro na ndege za kivita za Urusi ambazo zinatekeleza mashambulio dhidi ya waasi wanaompinga rais Assad.

Maafisa wa kampeni wa Bi Clinton wamemtuhumu Trump kwa kuwachezea Wamarekani kupitia wasiwasi wao.

Mgombea huyo ametishia kwamba hali mbaya zaidi itatokea iwapo mpango wa mpinzani wake wa chama cha Democratic wa kutaka kudhibiti anga ya Syria utatekelezwa.

Kwa upande mwingine Trump amewashambulia wafuasi na viongozi wa Republican ambao wamekataa kumuunga mkono katika mbio zake za kuwania urais.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *