Rais wa Marekani, Donald Trump amefafanua sababu ya kurejea kisa cha ukosefu wa usalama nchini Sweden alichosema kilitokea Ijumaa wakati hakukuwa na kisa kama hicho.

Akihutubia mkutano wa hadhara Jumamosi, alisema, “tazama yaliyotokea Sweden usiku wa kuamkia leo”, alipokuwa anataja maeneo ya Ulaya ambayo yamekumbwa na mashambulio ya kigaidi.

Trump aliandika kwenye Twitter baadaye Jumapili kwamba alikuwa akirejelea taarifa kwenye runinga huku akisema taarifa hiyo ilipeperushwa na kituo cha habari cha Fox News lakini hakusema ni lini.

Huenda alikuwa anarejelea makala iliyopeperushwa na Fox News Ijumaa usiku, ambayo iliangazia tatizo la wahamiaji na uhalifu nchini Sweden.

Licha ya kusema kisa “kilitokea usiku wa kuamkia jana Sweden”, msemaji wa White House Sarah Huckabee Sanders alisema kwamba Bw Trump alikuwa anazungumzia ongezeko la visa vya uhalifu kwa jumla na wala si kisa fulani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *