Rais wa Marekani, Donald Trump anatarajiwa kutia saini amri kuu kuweka masharti kuhusu wahamiaji wanaoingia nchini humo.

Taarifa kutoka Marekani inasema kuwa ataanza kwa hatua ya kuimarisha usalama katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico atakapozuru makao makuu ya wizara ya usalama wa ndani baadaye Jumatano.

Pia anatarajiwa kutoa tangazo la kuidhinisha sheria kali zaidi za kupata visa kwa wageni kutoka eneo la Mashariki ya Kati na Afrika ambayo yana Waislamu wengi.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Trump ameandika kwamba leo itakuwa siku muhimu sana kwa usalama wa taifa la Marekani.

Wakati wa kampeni yake ya urais, Donald Trump aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.

Aligusia ujenzi wa ukuta kati ya Mexico na Marekani kuzuia wahamiaji haramu na kuwapiga marufuku Waislamu kuingia katika taifa hilo kama sehemu ya vita dhidi ya ugaidi. Baadaye alibadili msimamo kidogo na kufafanua kwamba watakachofanyiwa Waislamu ni kufanyiwa ukaguzi mkali kabla ya kuruhusiwa kuingia Marekani.

Source: BBC

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *