Rais wa Marekani, Donald Trump amelihutubia Bunge la nchi hiyo kwa mara ya kwanza toka ashike wadhifa wa urais.

Hotuba yake kwenye Bunge hilo iliegemea zaidi katika maswala ya uhamiaji na kuwapunguzia kodi wananchi.

Lakini hotuba ya rais huyo wa Marekani haikugusia maswala ya soko la fedha kama ilivyotarajiwa na wawekezaji na wafanya biashara.

Katika hotuba yake aliwaambia wajumbe kwamba yuko tayari kwa mageuzi katika swala zima la uhamiaji. Hotuba yake ilionekana kuhama kwenye matamshi makali juu ya maswala ya uhamiaji ambayo alikuwa akiyatoa wakati wa kampeni.

Rais Trump alitolea mfano nchi kama Canada na Australia  ambazo alisema zina mifumo bora ya uhamiaji. Lakini baadhi ya wajumbe wa chama cha Republican wanapinga hatua anazotaka kuzichukua rais huyo wa Marekani kama kupunguza kwa kiwango kikubwa misaada ya Marekani kwa nchi za kigeni.

Kiongozi wa Seneti Mitch McConnell ambaye aliwahi kuongoza jopo lililosimamia bajeti ya misaada ya nje amesema haungi mkono kupunguza bajeti ya misaada ya nje.

Trump katika mpango wake analenga kupunguza misaada ya nje na badala yake kuiongezea wizara ya ulinzi kiasi cha dola bilioni 54.

Hatua hiyo itakuwa inapunguza kwa asilimia 37 fedha kutoka kwenye wizara za mambo ya ndani na ile ya diplomasia na mambo ya nje.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *