Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefunga maduka ya wafanyabishara mkoani Iringa wasiotumia mashine za kielektroniki za EFDs.
Hatua hiyo imekuja baada ya maofisa wa TRA kufanya ukaguzi wa kushitukiza katika maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa na kubaini uwepo wa wafanyabiashara wanaodaiwa kutokuwa na mashine za kutolea risiti za EFD.
Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Ndg Lampson Tulianje amesema wafanyabishara hao wamekaidi agizo la Serikali la kutakiwa kuwa na mashine kwa zaidi ya miezi mitatu.
Tulinje amefafanuaa kuwa lengo la kufikia hatua hiyo ni kuhimiza wafanyabiashara hao kulipa kodi stahiki kwa kutumia mashine hizo ambazo zina uwezo wa kuweka kumbukumbu vizuri za mauzo ya bidhaa zao.
Pia Tulinje ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuacha kushindana na Serikali badala yake kuhakikisha wananunua mashine hizo na kuzitumia kwa kuwa hata gharama wanazotumia zinarudishwa na TRA wakati wa kukadiria kodi zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabishara mkoani Iringa, Ndg Odilo Ngamiraga amesema wafanyabishara hawajagoma kutumia mashine hizo na kwamba tatizo lipo kwa wasambazaji ambao pindi wanapokwenda huambiwa wasubiri.