Mshambuliaji wa AS Roma, Francesco Totti ametokwa na machozi alipokuwa anaaga baada ya kucheza mechi yake ya mwisho katika klabu hiyo.

Mshambuliaji huyo wa umri wa miaka 40 amechezea klabu hiyo kwa miaka 25 toka aanze mpira.

Katika kipindi hicho chote Totti amefunga mabao 307 katika mechi 786 alizocheza ndani ya klabu hiyo katika mashindano tofauti.

Totti amecheza mechi ya mwisho dhidi ya Genoa ambapo Roma walishinda 3-2 kupitia bao la dakika ya mwisho la Diego Perotti ambalo liliwahakikishia nafasi ya kucheza hatua ya makundi Klabu Bingwa Ulaya.

Baada ya mechi, Totti alisoma barua kwa mashabiki, na kusema: “Naogopa. Sijui siku za usoni zitakuwaje.”

“Tafakari, kwamba wewe ni mtoto na umo katikati ya ndoto nzuri…na mamako anakuamsha uende shuleni.

“Unajaribu kurejea kwenye ndoto yako…unajaribu sana lakini huwezi.

“Wakati huu si kwamba ni ndoto, ni uhalisia. Na siwezi kurejea tena.”

Anatarajiwa kuwa mkurugenzi katika klabu ya Roma lakini kumekuwepo na taarifa kwamba huenda akaelekea kwingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *