Beki wa kimataifa wa Ivory Coast, Serge Aurier anatarajia kukamilisha usajili kujiunga na Tottenham akitokea Paris St-Germain.

Mkataba wa uhamisho wake wa karibu £23m umecheleweshwa na matakwa kuhusu kibali cha kufanyia kazi Uingereza.

Changamoto zilizuka kwa sababu mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ivory Coast mwenye miaka 24 ana hukumu iliyoahirishwa kwa sababu ya kosa la kumshambulia afisa wa polisi mjini Paris mwaka jana.

Hata hivyo, taarifa zinasema tatizo hilo limetatuliwa na Spurs wanaweza kuendelea na utaratibu wa kumchukua beki huyo wa kulia.

Atakuwa mchezaji wa nne kununuliwa na Spurs majira ya sasa ya joto, baada ya beki Juan Foyth, golikipa Paulo Gazzaniga na beki wa kati Davinson Sanchez aliyenunuliwa kwa rekodi ya klabu hiyo ya £42.

Kyle Walker, 27, aliuzwa Manchester City kwa £50m mwezi Julai naye beki wao Kevin Wimmer akajiunga na Stoke City kwa £18m.

Aurier alijiunga na PSG kutoka Toulouse, awali kwa mkopo mwaka 2014, kabla ya kuhamia Paris kwa mkataba wa kudumu mwaka 2015.

Alianza kila mechi timu ya taifa ya Ivory Coast iliposhinda Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2015, ambapo alifunga mkwaju wa penalti wakati wa matuta dhidi ya ghana kwenye fainali.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *