Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa mwezi huu Novemba kuwa kutakuwa na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi.

Hivyo , maeneo mengi ya nchi yanatarajia kupata mvua chini ya wastani, hasa maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria yatapata mvua za wastani na chini ya wastani.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agness Kijazi amesema kuwa upungufu huo wa mvua, unatokana na kuwepo kwa viashiria vya La Nina ambapo maeneo ya bahari ya Pasific pamoja na magharibi mwa bahari ya Hindi, hali ya joto la bahari linaonekana kushuka na kuwa chini ya wastani.

Dk Kijazi amesema kipindi cha mwezi Oktoba mwaka huu, mvua zilichelewa kuanza katika maeneo mengi yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka, hali iliyosababisha upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika maeneo mengi ya nchi.

Amesema takwimu zinaonesha kuanzia mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu hadi sasa, kumekuwa na hali ya upungufu wa mvua na kusababisha hali ya mtawanyiko wake kuwa hafifu katika maeneo mengi.

Amesema mwezi Septemba mwaka huu, walitoa utabiri wa msimu wa hali ya mvua za vuli kwa maana ya Oktoba, Novemba na Desemba na utabiri huo ulionesha katika maeneo mengi ya nchi zitapata mvua chini ya wastani na hii ni kutokana na hali ya La Nina inayoendelea.

Amesema mamlaka hiyo inaendelea kufutilia mifumo ya hali ya hewa na kuweza kutoa mrejesho wa hali ilivyo, kuonesha hali gani ilivyokuwa Oktoba na Novemba, ambapo hakuna matarajio ya kuwa na mvua katika maeneo mengi ya nchi.

Amewashauri wakulima kupata ushauri wa maofisa ugani, ambao wataweza kuwashauri vizuri juu ya taratibu ambazo wataweza kuzitumia katika kipindi hiki cha mvua za vuli katika kilimo chao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *