Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wamekamata lori lililokuwa likisafirisha mbao zilizovunwa kinyume cha sheria baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Lori hilo lenye namba za usajili T 676ANQ aina ya Scania lililokuwa likitoka Kigoma kwenda jijini Dar es Salaam, lilikutwa limetelekezwa katika maegesho ya mkazi wa Dar es Salaam, eneo la Amana katika Manispaa ya Ilala na dereva wa lori hilo kutokomea kusikojulikana.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kuzibaini mbao hizo kutokana na kufunikwa kwa miche ya sabuni, viroba vya dawa za kuku pamoja na chupa tupu zilizokuwa zimeshatumika.

Kaimu Ofisa Habari ambaye pia ni Ofisa Misitu Mkuu wa Wakala hao, Nurdin Chamuya alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria kuwa kuna lori limebeba mbao zilizovunwa kiharamu, walishirikiana na kikosi maalumu dhidi ya ujangili wa wanyama pori na kubaini lori hilo likiwa limetelekezwa katika eneo hilo.

Amesema wanamtafuta dereva wa lori hilo pamoja na mmiliki wake ili sheria ichukue mkondo wake huku akitoa mwito kwa wananchi kufuata taratibu na sheria za uvunaji wa miti ya mbao ikiwa ni pamoja na kuwa na vibali halali vinginevyo atakayebainika atashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *