Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema hadi sasa linamtambua Kocha wa Azam FC, Zeben Hernandez, kufuatia kupokea kibali chake cha kufanya kazi nchini huku wakiwa hawatambui uwepo wa kocha, Joseph Omog wa Simba kutokana na kibali chake kutowasili katika shirikisho hilo.

TFF pia imezitaka klabu zote za ligi kuu kuwasilisha nakala tatu za usajili wa kila mchezaji ili kuweza kutambuliwa kabla ya kuupitisha usajili huo.

Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, amesema kabla dirisha la usajili halijafungwa, klabu zote zinatakiwa kuwasilisha vibali vya usajili wa wachezaji ili vihakikiwe na iwapo kibali cha mchezaji yeyote hakitafika, basi hatapata nafasi ya kucheza.

Lucas amesema kwamba wameamua kutumia kanuni ya 67 kifungu cha 1, 2 na 8 katika kuhakikisha klabu zote za ligi kuu zinawasilisha nakala za usajili wa wachezaji wao ambapo zinatakiwa kuwa tatu na kila mchezaji wa ligi kuu atalipiwa kiasi cha shilingi 50,000 na wa Ligi Daraja la Kwanza shilingi 25,000.

Kwa upande wa makocha, hadi sasa kocha ambaye kibali chake kimewasili TFF ni wa Azam pekee na kwa upande wa mchezaji wamepokea kibali cha Obrey Chirwa wa Yanga na dirisha la usajili litafungwa Agosti 6, mwaka huu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *