Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amelitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na wadau wengine kushirikiana kwa hali na mali kuhakikisha wanadhibiti bidhaa hafifu na duni zinazoingizwa na zinazotengenezwa nchini.

Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mtaka katika Mkutano wa Nne wa Wadau wa Kudhibiti Viwango unaofanyika hapa, Gambo alisema nchi inakabiliwa na janga kubwa la kuzagaa kwa bidhaa duni na hafifu zisizo na viwango na kwa kiasi kikubwa inachangia umasikini kwa wananchi wake.

Amesema hilo linapaswa kudhibitiwa kwa nguvu zote kwa wadau wa sekta hizo pamoja na wananchi kwa kuwafichua wahusika, na TBS na wadau wengine, wanapaswa kushirikiana kwa hali na mali kukabiliana na hali hiyo ili Tanzania isiwe dampo la bidhaa zisizo na viwango.

Pamoja na kutoa mwito kwa TBS na wadau wengine, Gambo aliwataka Watanzania kususa bidhaa hafifu na duni, kwani ndio njia pekee ya kuua soko la bidhaa hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *