Jeshi la Polisi Kanda maalumu ya Tarime na Rorya mkoani Mara limeteketeza mashamba ya bangi yenye ukubwa wa ekari 120 ambayo yamelimwa katika maeneo tofauti mkoani humo.

Operesheni ya kuteketeza mashamba hayo yamefanywa kwa kushirikiana kati ya jeshi la polisi na watendaji mbali mbali wa Serikali ya Wilaya ya Tarime hapo jana.

Mkuu wa wilaya ya Tarime ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo, Glorious Luoga amesema kuwa zoezi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa na litakuwa endelevu ili kupambana na kilimo hicho haramu cha bangi.

Kwa upande wake Afisa Tarafa wa Inano ndani ya Wilaya hiyo, Chacha Marwa amesema kuwa wamebaini kuwa kila kaya ndani ya kitongoji cha Kelenge inamiliki shamba la Bangi ambapo mashamba mengi yapo pembezoni mwa mto.

Wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo ya Tarime wamesema kuwa wamesikitishwa na baadhi ya wananchi kutumiwa na wafanyabiashara wa nje ya nchi kulima zao hilo haramu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *