Benki ya Dunia inatarajia kuipatia Tanzania ruzuku na mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.6 (Sh trilioni 3.5).

Fedha hizo ni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo nishati ya umeme, kilimo biashara na ukarabati wa miundombinu ya Reli ya Kati.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu amesema jijini Washington DC nchini Marekani ambako ujumbe wa wataalamu wa masuala ya uchumi na fedha kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wanashiriki Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Pia amesema Benki ya Dunia imesifu hatua zilizofikiwa na serikali ya Tanzania katika kukuza na kusimamia uchumi wake, ambao licha ya uchumi wa dunia kushuka viwango vyake vya ukuaji uliotarajiwa wa asilimia 3.3 na kukua kwa asilimia 1.5 tu, uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya asilimia 7.

Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, amesema kuwa mkopo utakaotolewa ni pamoja na dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya kulijengea uwezo Shirika la Umeme (Tanesco) ili liondokane na nakisi, inayosababishwa na madeni makubwa yanayolikabili.

Dk Mpango alifafanua kuwa mkopo huo, pia utaiwezesha serikali kulipa madeni inayodaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii baada ya kufanyika kwa uhakiki wa kina wa madeni hayo ili kuiwezesha mifuko hiyo, itoe huduma inayostahili kwa wanachama wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *