Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Tanzania ipo tayari kutoa walimu wa kwenda kufundisha lugha ya Kiswahili nchini Rwanda.

Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli amechukua hatua hiyo, baada ya Rwanda kuamua Kiswahili kianze kufundishwa katika shule zake.

Rais alisema hayo alipopokea barua yenye ujumbe wa Rais Paul Kagame wa Jamhuri wa Rwanda, iliyowasilishwa kwake na Mjumbe Maalumu ambaye ni Waziri wa Elimu wa Rwanda, Dk Musafiri Malimba.

Pamoja na kupokea barua hiyo, Rais Magufuli na Dk Malimba walizungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda, ikiwemo katika sekta ya elimu hususani maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Magufuli aliipongeza Rwanda kwa kuamua lugha ya Kiswahili kianze kufundishwa katika shule zake na alisema Tanzania ipo tayari kutoa walimu wa kwenda kufundisha lugha hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *