Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amewahakikishia wananchi wa Mbeya kwamba Bunge la bajeti litakaloanza vikao vyake mwaka huu, limejipanga katika kupitisha bajeti rafiki itakayosaidia kupunguza makali ya maisha ya Watanzania.

Sugu aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Jiji la Mbeya katika viwanja vya mikutano vya Shule ya Msingi ya Mwenge, eneo la Soweto jijini hapa.

Amesema Bunge limejipanga katika kusimamia uchumi wa nchi pamoja na masilahi ya Watanzania hasa katika suala zima la ajira na biashara kwa wajasiriamali.

Amesema bajeti rafiki ndiyo inayohitajika kwa Watanzania kuweza kutoa ajira kwa vijana na kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira za Serikali ambazo hadi sasa Serikali imesimamisha zoezi hilo na kuwafanya wahitimu wa vyuo kuendelea kubaki mitaani.

Mbunge huyo aliongeza kwamba kwa hali ya nchi ilipofikia, ni mbaya hivyo wao kama wabunge wataangalia njia mbadala ya kuishauri Serikali.

Hata hivyo, Sugu aliwataka wakazi wa Jiji la Mbeya hasa vijana kubadilika na kuachana na tabia za kuwashabikia viongozi ambao wamekuwa wakiendesha mambo kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *