Muigizaji wa Bongo movie, Steven Mengere ’Steve Nyerere’ amesema ni lazima watawafunga wasanii wa muziki wa Bongo Fleva katika mechi maalum ya kuchangia fedha kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera, hivi karibuni.

Mbali na mechi hiyo, pia kutakuwa na mechi kati ya timu ya soka ya wabunge wa Simba dhidi ya wa Yanga, pamoja na mechi ya netiboli ya Bunge itakayoumana na ile ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Mechi hizo zote zitapigwa Jumapili ya Septemba 25, mwaka huu kwenye uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Steve Nyerere ameyasema hayo alipozungumza na wanahabari kwenye mkutano uliokuwa umeandaliwa na Kampuni ya Tanzania Sisi Nyumbani (TSN) ambayo ndiyo imedhamini mechi hiyo ya Bongo Muvi dhidi ya Bongo Fleva.

Akizungumza katika mkutano huo,Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Biashara wa TSN, Jahu Mohamed, alisema TSN imejitokeza kudhamini mechi hiyo kutokana na kuguswa na janga hilo na kuona ni vyema kushirikiana na wasanii hao ili kuhamasisha uchangiaji wa pamoja.

Aliongeza kuwa, mbali na kudhamini mchezo huo,pia tayari wametoa mchango ambao tayari wameupeleka kwa waathirika wa tetemeko hilo.

Katika mchezo huo, viingilio vitakuwa ni Sh 3,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, Sh 10,000 na 15,000 itakuwa kwa ajili ya viti vya rangi ya machungwa huku Sh 50,000, 100,000 na 200,000 ikiwa ni kwa V.I.P C, B na A.

Lakini kwa viti 50 pekee maalum vitakavyokuwa karibu na mgeni rasmi wa mechi hiyo ambaye atatajwa baadaye, kila kimoja kitalilipiwa Sh 1,000,000.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *