Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema serikali imewekeza Sh bilioni 37 kwa ajili ya miundombinu ya majengo katika Chuo cha Serikali za Mitaa kilichopo Hombolo Dodoma na sasa wanaangalia namna ya kuongeza watumishi chuoni hapo.

Jafo amesema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya utawala na serikali za Mitaa chuoni hapo ambapo ilitembelea miundombinu ya chuo ikiwemo mabweni, madarasa, maktaba, zahanati na nyumba za watumishi.

Jafo amesema serikali ilifanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ili chuo hicho ambacho kimekuwa kikipokea wanafunzi wa ndani na nje ya nchi kiwe na mazingira bora. Jafo alisema wataangalia jinsi ya kufanya ili kuongeza watumishi kwani sasa kuna upungufu wa watumishi 101.

Kwa upandande Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Chuo hicho, Profesa Suleiman Ngwale aliwataka Wazanzibari kujiunga na chuo hicho na kuongeza kuwa haoni kwa nini Wazanzibari hawasomi katika chuo hicho cha serikali za mitaa licha ya Zanzibar kuwa na halmashauri.

Mwenyekiti wa kamati ya bunge ya utawala na serikali za mitaa Jason Rweikiza alisema lengo la ziara hiyo ni kujifunza na kuona chuo hicho kinafanya nini. Mbunge wa Viti Maalumu, Angelina Malembeka alisema sasa ni wakati wa Wazanzibari kutumia chuo hicho kupata ujuzi mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *