Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa na Spika wa Bunge la Afrika Mashariki, Daniel Kidega kwa kazi kubwa ya kujenga uchumi wa Tanzania.

Spika huyo amewaomba wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki kuunga mkono jitihada zinazofanywa na kiongozi huyo.

 Kidega amesema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kukutana na Dk Magufuli na kufanya naye mazungumzo yaliyojikita kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwemo kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya nchi wanachama, kuinua hali ya uchumi na kutatua matatizo yanayozikabili baadhi ya nchi wanachama wa jumuiya.

Pia Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini, Sarah Cooke ambapo viongozi hao wamezungumzia namna Tanzania na Uingereza zitakavyoimarisha uhusiano na ushirikiano katika uwekezaji na biashara, mapambano dhidi ya Rushwa na dawa za kulevya, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuimarisha huduma za usafiri wa anga.

Dk Magufuli amemshukuru Balozi Cooke na kumhakikishia kuwa Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na uhusiano wake wa kihistoria na Uingereza katika kujenga uchumi imara wa Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *