Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amewataka wakuu wa mikoa na wa wilaya kupita darasani kukagua wanachofundisha walimu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu iliyokusudiwa na serikali.

Akizungumza na wakazi wa vijiji vya Wotta na Wangi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Simbachawene amesema viongozi hao wana jukumu kubwa la kufuatilia maendeleo ya wanafunzi ili baadaye waweze kutoa ushauri na si kuwaachia jukumu hilo wakaguzi pekee.

Aidha, ameaziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini hususan halmashauri zihakikishe zinashirikiana kukagua miradi inayohusu maendeleo ya elimu ili kuona kuwa inakidhi ubora kulingana na gharama iliyotolewa.

Amesema kila mwezi Serikali hutoa Sh bilioni 23 kwa ajili ya uendeshaji shule na pia kuanzia Agosti, mwaka huu, serikali imekuwa ikiwapa walimu wakuu wa shule za msingi Sh 200,000 kwa mwezi, kwa ajili ya kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana shuleni.

Amesema viongozi wa halmashauri hawana budi kupita katika shule hizo ili kuona mapungufu yanayoweza kujitokeza katika baadhi ya shule.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *