Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene amesema ni wakati wa wananchi wa Dodoma kufurahi kwani tangu walipoahidiwa kuletewa Serikali mwaka 1973 hawakuwahi kuandamana kuidai hadi Mungu alipopenda iwe hivyo.

Amesema hayo juzi wakati wa kumkaribisha Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa nyumbani kwake Mlimwa baada ya kuwasili rasmi kuhamia mkoani Dodoma. Simbachawene alisema wananchi wa Dodoma ni wapole, wasikivu na wakweli katika vitendo.

Simbachawene amesema ilizoeleka kusikika kuhamia Dodoma ni ndoto lakini sasa imetimia na Dodoma ni makao makuu ya nchi. Alisema sababu ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi ni ya msingi kutokana na kuwa katikati ya nchi.

“Tutakuwa si wenye fadhila kama hatutaishukuru serikali ya Awamu ya Tano, sasa biashara zitachangamka kutokana na ujio wa Makao Makuu, Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA), ndio wameifanya Dodoma iliyopo leo,” alisema.

Katika mapokezi hayo nyumbani kwa Waziri Mkuu, alikabidhiwa funguo na Meya wa Manispaa ya Dodoma, Jafar Mwanyemba, kama ishara ya kumkaribisha kuwa mwenyeji wa mkoa wa Dodoma. Vile vile alivalishwa vazi la kimila la mgolole na kukabidhiwa fimbo. Akitoa salamu za wazee, Balozi mstaafu, Job Lusinde, alisema hayawi hayawi sasa yamekuwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *