Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene amemtumbua Ofisa Elimu Msingi, Scolastica Kapinga, kutokana na kutopeleka walimu katika Shule ya Msingi Mbalawala, iliyopo Manispaa ya Dodoma.

Hatua hiyo imechukuliwa siku chache baada ya wazazi kulazimika kuifunga shule hiyo ambayo inadaiwa kuwa na wanafunzi 922 na walimu watatu.

Waziri Simbachawene alisema Serikali haiwezi kumvumilia ofisa elimu huyo ambaye ameshindwa kusimamia sekta ya elimu.

Kutokana na hali hiyo, Simbachawene alimwagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Godwin Kunambi, kupeleka walimu 10 shuleni hapo, ndani ya wiki mbili.

Kwa upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde amesema ukosefu wa walimu umekuwa ni changamoto kwao na kwamba zinahitajika nguvu za ziada kuwa na idadi kubwa ya walimu.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Cristina Mndeme amesema suala la idadi ya walimu linatakiwa kuangaliwa kwa umakini kwani linaathiri masomo ya wanafunzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *