Shirika la ndege la Emirates limetangaza kupunguza safari za ndege katika miji mitano nchini Marekani kuanzia mwezi ujao.

Shirika hilo la ndege la Dubai limesema mabadiliko hayo yanatokana na kushuka kwa idadi ya watu wanaosafiri kwenda Marekani.

Hatua hii inatokana na marufuku iliyowekwa na serikali ya Rais Donald Trump kuzuia baadhi ya raia wa mataifa yenye Waislamu wengi kuzuru Marekani, pamoja na masharti mengine makali ya kiusalama.

Mwezi Machi, Marekani ilipiga marufuku vifaa vya kielektroniki ambavyo ni vikubwa kuliko simu za rununu visibwebwe kwenye sehemu ya mizigo ya ndege kutoka viwanja 10 vya ndege.

Viwanja hivyo ni pamoja na vya Dubai, na mataifa mengine ya Mashariki ya Kati, Afrika kaskazini na Uturuki.

Rais Trump pia alitia saini amri ya kuwazuia wahamiaji na raia kutoka mataifa kadha yenye Waislamu wengi kutoka Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika wasizuru Marekani.

Kwa upande wa Rais wa Emirates, Tim Clark alisema mwezi jana kwamba idadi ya watu wanaotaka kwenda Marekani imeshuka kwa theluthi moja tangu kutolewa kwa tangazo la Bw Trump.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *