Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema iwapo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) litaikatia umeme Zanzibar kutokana na deni wanalodaiwa, wataweza kurudi katika matumizi ya asili ambayo ni kutumia vibatari kupata mwanga.

Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amaan Abeid Karume, akitokea nchini Indonesia katika mkutano maalumu aliomuwakilisha Rais Dk. John Magufuli.

Kauli hiyo imekuja wakati Tanesco jana ikiwa imetoa siku 14 kwa wadaiwa wote sugu, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), linalodaiwa Sh bilioni 127, kulipa deni hilo ndani ya muda huo kabla ya kukatiwa umeme.

Wiki iliyopita, Rais Magufuli aliiagiza Tanesco kukata umeme kwa wadaiwa wote sugu, akisema hata kama Ikulu ya Magogoni inadaiwa, nayo pia ikatiwe nishati hiyo.

Jana mara baada ya Dk. Shein kuwasili, alizungumzia mafanikio ya safari yake ikiwa ni pamoja na mipango ya viwanda, kauli iliyofanya waandishi kuuliza viwanda hivyo vitaendeshwa vipi ilihali Tanesco imetangaza kuikatia umeme Zanzibar.

Amesema akiwa safarini alisoma magazeti mawili yaliyoandika juu ya Zanzibar kukatiwa umeme, lakini haamini kama taarifa hizo zina ukweli, huenda waandishi walinukuu vibaya vyanzo vya taarifa hiyo.

Alisema atashangazwa iwapo umeme utakatwa, ikizingatiwa mahusiano mazuri yaliyopo baina ya pande mbili hizi zinazounda Tanzania.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *