Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein amevitaka vyuo vikuu nchini kusajili wa wanafunzi wenye sifa za kitaifa na kimataifa.

Ameyasema hayo jana katika Chuo Kikuu cha Zanzibar kilichopo Tunguu, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja katika katika Mahafali ya 14 ya chuo hicho.

Amesema hivi karibuni kumeibuka baadhi ya vyuo vinavyosajili wanafunzi bila ya kufuata viwango husika, jambo ambalo linaharibu sifa ya elimu na maendeleo ya wananchi na nchi kwa jumla, itakayoweza kusababisha kupata wataalamu wasiokuwa na sifa hapo baadaye.

Amesema kuwepo kwa ushindani mkubwa wa kutafuta wanafunzi wapya wanaotaka kujiunga katika vyuo vya ndani na nje ya nchi isiwe sababu ya kuharibu ubora wa elimu kwa kusajili wanafunzi wasio na viwango kuingia katika vyuo vikuu.

Aidha, alivitaka vyuo vikuu nchini kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakuwa na wahadhiri na vifaa vya kutosha sambamba na kuwa na uwezo wa kuendesha mafunzo hayo ili kuepuka kutoa elimu isiyokidhi haja.

Amesema mambo hayo kwa pamoja ni muhimu katika kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa Tanzania.

Amesema ubora wa elimu inayotolewa ni suala la ushirikiano kati ya jamii, vyuo na serikali na kuhimiza haja kwa vyuo vikuu vya Zanzibar kufanya kazi karibu zaidi katika kuhakikisha elimu inakidhi mahitaji yaliyokusudiwa na wanafunzi nao wanakidhi viwango.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *