Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein ameitaka Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira kuongeza kasi ya kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria ya ardhi hasa kuanzia umiliki hadi matumizi yake ili wananchi wapanue uelewa wao kuhusu suala hilo.

Amesema ardhi kwa Zanzibar ni suala lenye umuhimu wa kipekee na wakati wote Serikali kupitia wizara husika hujikita kuwaeleza wananchi mipango na hatua mbalimbali inazozikusudia kuzifanya kuwawezesha kwenda sambamba na mipango ya serikali.

Dk Shein ametoa agizo hilo wakati wa kikao cha kujadili utekelezaji wa mpango kazi wa Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira, kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016-2017, kilichofanyika jana Ikulu, Zanzibar.

Ameiagiza wizara hiyo kukagua maeneo mbalimbali yasiyotumika na kuyapima kwa lengo la kuyahifadhi, ili kuepuka matumizi yasiyostahili.

Aliutahadharisha uongozi wa wizara hiyo kuwa hatua za haraka zinahitajika kutekeleza mipango ya matumizi ya ardhi, kwa kuwa wananchi kamwe hawataisubiri. Badala yake alisema kuwa wataendelea kutumia ardhi kwa mujibu wa mahitaji yao yanayoweza kuwa kinyume na mahitaji, malengo na mipango ya Serikali.

Kuhusu migogoro ya ardhi ambayo inasababisha kuwepo kwa kesi nyingi katika Mahakama ya Ardhi, Dk Shein alitoa mwito kwa wizara hiyo kuharakisha mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria Namba 7 ya Mwaka 1994 na marekebisho yake ya Sheria Namba 1 ya Mwaka 2008 ya Mahakama ya Ardhi ambayo inadaiwa kuwa chanzo cha kesi nyingi za ardhi kuchukua muda mrefu kuhitimishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *