Serikali imetoa vigezo vitakavyozingatiwa katika utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo wa 2016/2017.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya amesema Dar es Salaam kuwa vigezo hivyo vinazingatia Dira ya Taifa 2025, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Sera ya Elimu na Mafunzo (2014) na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Waziri huyo amesema serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, imekuwa ikiwakopesha wanafunzi wenye sifa za kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini kugharamia masomo yao.

Amesema katika utekelezaji wa jukumu hilo, Serikali huandaa sifa na vigezo vya utoaji mikopo kila mwaka ili kuendana na malengo na matarajio yaliyopo katika mipango na mikakati ya kitaifa kama ilivyoainishwa katika mipango mbalimbali. Alisema kwa kuzingatia mipango mikakati na sera hizo, pia Mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka 2016/2017 katika mwaka wa masomo 2016/17 umetolewa.

Waziri Manyanya alisema vipaumbele vingine ni Uhandisi wa Viwanda, Kilimo, Mifugo, Mafuta na Gesi Asilia, Sayansi Asilia na Mabadiliko ya Tabianchi na Sayansi za Ardhi, Usanifu Majengo na Miundombinu.

Ameeleza vipaumbele vingine kuwa ni uhitaji wa waombaji hususani wenye mahitaji maalum kama vile ulemavu na uyatima na ufaulu wa waombaji katika maeneo ya vipaumbele na umahiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *