Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema wizara yake inakusudia mpaka Juni 2017 iwe imetoa takribani hati laki nne, hivyo kushauri kasi katika upimaji ardhi.

Ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wapima Ardhi Tanzania (IST) Alisema utoaji wa hati hizo utatokana na kasi ya wapima ardhi katika maeneo yakiwemo mashamba, viwanja na majengo.

Pia amewataka wapimaji hao kuja na mapendekezo ni namna gani wanaweza kuangalia gharama za upimaji wa ardhi ili kuwezesha watanzania wengi wanapimiwa ardhi zao, kwa kuwa upimaji wa ardhi unasaidia kuchangia kukua kwa pato la ardhi kila mwaka.

Pia ameiagiza IST iweke mkakati maalumu wa kujenga utaratibu wa kudhibiti maovu yote katika taaluma hiyo kwa kutoa ushirikiano wa kutosha serikalini, lakini pia isaidie kutoa ufafanuzi wa mwenendo wa taaluma na wataalamu wa upimaji ardhi inapotokea sintofahamu miongoni mwa wadau mbalimbali wa wapima ardhi wanapotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa miiko na maadili ya taaluma hiyo.

Naye Rais wa IST, Martins Chodota amewataka wapima ardhi watambue umuhimu wao na majukumu yao na kuacha kufanya kazi kwa kuharibu na kusababisha migogoro ya ardhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *