Shamba lililokuwa linamilikiwa na Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, lililopo Mabwepande limefutiwa hati zake na umiliki umerudishwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ambayo itafanya utaratibu wa kupima viwanja na kuwagawia wananchi waliohusika kwenye mgogoro huo.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi zaidi ya 250 kulalamikia unyanyasaji wanaofanyiwa kupitia shamba hilo, na Mkuu wa Wilaya hiyo, Ally Hapi kupeleka malalamiko hayo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo Rais John Magufuli aliidhinisha kufutiwa hati kwa shamba hilo.
Akizungumza na wananchi wa kata hiyo ya Mabwepande jana, Hapi alisema shamba hilo lenye ekari 33 limefutiwa hati zake tangu Oktoba 28, mwaka huu na kwamba tayari Sumaye ameandikiwa barua ya kutojihusisha na shamba hilo baada ya kushindwa kukidhi masharti ya kisheria.
Ameongeza kuwa wananchi hao waliokuwamo kwenye mgogoro ambao wataonekana wana vigezo vya kupatiwa viwanja, watafikiriwa kwa masharti ambapo baada ya kupimwa viwanja hivyo watawekewa gharama nafuu kwa ajili ya wao kununua.
Pia amesema, wananchi hao wenye makazi ya kudumu kwenye eneo hilo, watahakikiwa ili kuepusha watu wasiokuwamo kujiingiza kwa lengo la kuonekana nao walikuwa sehemu ya tukio.
Hata hivyo alisema wataendelea kutoa taarifa kwa Rais kuhusu maeneo ambayo wananchi wanayahodhi bila ya kuyafanyia kitu chochote ili nayo yafutiwe hati.