Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema katika kipindi cha miezi mitatu imevuka malengo ya ukusanyaji wa mapato ambapo imekusanya Sh bilioni 117.66 sawa na asilimia 99.5 ya malengo yaliyowekwa.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Khalid Salum Mohamed amesema wamevuka malengo yaliyowekwa na kuifanya serikali kumudu kutekeleza na kusimamia majukumu yake kikamilifu ikiwemo kutoa huduma za jamii za afya na elimu.

Dk Mohamed amesema makusanyo ya Juni yamevuka malengo na kuvunja rekodi ambapo kabla ya hapo makusanyo ya kodi yalikuwa yamefikia Sh bilioni 82.45.

Alisema kwamba mapato yamekuwa kwa asilimia 42.7 kutoka Sh bilioni 82.45 hadi kufikia Sh bilioni 117.66.

Waziri huyo pia amesema ongezeko kubwa limeripotiwa katika Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ambayo imekusanya Sh bilioni 36.04 hadi kufikia Sh bilioni 56.72 wakati Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 37.1 hadi kufikia Sh bilioni 49.8.

DK Mohamed aliongeza kwa kusema kutokana na serikali kumudu kukusanya mapato yake vizuri katika sekta zote, imefanikiwa kulipa mishahara kwa wakati kwa watumishi wote wa serikali na taasisi zake ikiwemo mashirika ya umma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *