Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kutafuta fedha za mafunzo kwa ajili ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini ili kuziba pengo la wahadhiri waandamizi lililopo hivi sasa.

Waziri Mkuu  pia amevitaka vyuo hivyo viweke utaratibu wa kuachiana nafasi ama kurithishana kazi (succession plan).

 

Amesema yeye binafsi anatambua upungufu uliopo umesababishwa na masharti ya ajira za mkataba kwa wahadhiri waandamizi kuwa miaka 65 na maprofesa kuwa miaka 70.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Oktoba 25, 2016) wakati akifunga kilele cha maadhimisho ya miaka 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyoanza jana kwenye ukumbi wa Nkrumah. Kampasi ya Mwalimu J. K. Nyerere, jijini Dar es Salaam.

 

Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi wa vyuo hivyo, kikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kuhakikisha inaondoa malimbikizo ya madai kwa watumishi wote wa umma na hivi sasa inakamilisha uhakiki wa taarifa za kiutumishi kwa watumishi wa umma ili kubaini watumishi hewa.

 

Akifafanua kuhusu mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kufanya uhakiki wa taarifa za waombaji wa mikopo. Ametoa wito kwa wanufaika na waombaji wote wa mikopo wahakikishe kuwa wanatoa taarifa zilizo sahihi na za uhakika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *