Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema serikali inajipanga kuondoa utitiri wa kodi mbalimbali zinatozwa kwenye viwanda kama hatua ya kuviwezesha viwanda vingi nchini kuongeza uzalishaji na kutoa ajira nyingi kwa Watanzania.

Makamu huyo wa Rais ametoa kauli hiyo jana jijini Arusha baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza mafuta ya kula cha Mount Meru Millers kujua changamoto zinazokikabili ili serikali izifanyie kazi kwa lengo la kuleta nafuu kwenye uzalishaji wa mafuta ya kula nchini.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Samia alisema mlolongo wa kodi zinazotozwa kwa wamiliki wa viwanda hazina uratibu mzuri hivyo mkakati wa serikali ni kuweka utaratibu mzuri wa ulipaji wa kodi hizo ikiwemo kuondoa zilizo kero katika viwanda.

Amesisitiza kuwa serikali imedhamiria kuhakikisha viwanda vingi vinajengwa nchini na kutumia malighafi zinazozalishwa nchini, hali itakayosaidia uuzaji wa bidhaa zinazozalishwa Tanzania kuuzwa kwenye masoko ya nje, hivyo kuliingizia taifa mapato na kuongeza ajira.

Samia alisema ziara anazozifanya kwenye viwanda mkoani Arusha zinamuwezesha kujionea jinsi vinavyofanya kazi za uzalishaji, ikiwa ni pamoja na kuzijua changamoto zinazokwamisha ufanisi wa viwanda hivyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Mount Meru Millers, Atul Mittal, alisema kama serikali itafuta au kuondoa utitiri wa kodi wanazotozwa wenye viwanda hivyo watakuwa na uwezo wa kuongeza uzalishaji na kutoa ajira nyingi kwa Watanzania.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *