Serikali imewatoa wasiwasi wakazi na wafanyabishara wa Kanda ya Ziwa Victoria kuwa iko katika hatua za mwisho za kukamilisha taratibu za ujenzi wa meli mpya kubwa na ya kisasa ambayo itakuwa na uwezo wa kuchukua mizigo tani 300, magari 25 na madaraja matatu kwa ajili ya sehemu ya kukaa abiria.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua bandari ya Bukoba, mkoani Kagera, Waziri Profesa Mbarawa amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo umechelewa kutokana na kukosa sifa kwa Makandarasi wawili waliojitokeza mwanzoni kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa ujenzi.
Aidha, Waziri Mbarawa amefafanua kuwa kutokana na utendaji mbovu wa bandari hiyo anatarajia kuleta wafanyakazi makini kwa ajili ya kupitia taaria za kifedha za utoaji na usafirishwaji wa mizigo bandarini hapo.
Naye, Meneja wa Mamlaka ya Bandari Kanda ya Ziwa, Bw. Abel Moyo ameiomba Serikali kufanya ukarabati wa Meli nchini hasa zilizopo Kanda ya Ziwa ili kuweza kuondoa adha wanazozipata wakazi wa mikoa hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua Shirika la Posta mkoani humo na kuahidi kupeleka wakaguzi wa ndani kwa ajili ya kukagua na kujiridhisha juu ya mapato na matumizi ili kubaini ubadhilifu unaofanywa na watendaji wa Posta.