Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itahakikisha inajenga barabara za viwango vya kimatiafa ili kurahisisha usafiri kwa wananchi.

Majaliwa amesema hayo leo wakati akizumngumza na wananchi wa Tengeru, wilayani Arumeru, mkoani Arusha mara baada ya kukagua barabara ya Sakina-Tengeru yenye urefu wa km. 14.1 ambayo itakuwa na njia nne za magari.

Amesema kuwa maboresho ya barabara za Jiji la Arusha yanafanyika ili kuwezesha wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi na viwanda vitakapoanza kujengwa, hapatakua na shida ya mawasiliano.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Eng. Mgeni Mwanga alisema ujenzi wa barabara hiyo ambao ulianza Juni 2015, unatarajia kukamilika Juni 2018.

Pia Eng. Mwanga amesema mkandarasi wa barabara hiyo ataanza kujenga barabara nyingine ya km. 42.1 inayoanzaia Usa River hadi Kisongo kwa kiwango cha lami ambayo itakuwa na madaraja saba wakati ile ya Sakina hadi Tengeru ina madaraja makubwa mawili yatakayokuwa na uwezo wa kupita hata magari makubwa.

Naye mbunge wa Arumeru Mashariki, Bw. Joshua Nassari alisems uhaba wa ardhi bado ni tatizo kubwa kwenye wilaya hiyo kiasi kwamba hawana hata eneo la kujenga shule au zahanati.

Kutokana na malalamiko  hayo kutoka mbunge Nassari, Waziri Mkuu amemuagiza mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aendelee na zoezi la kuuzungukia mkoa wake ili kubaini maeneo yenye matatizo ya ardhi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *