Timu ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys leo inatarajiwa kwenda Congo Brazzaville tayari kwa kuwavaa vijana wa huko mwishoni mwa wiki hii.

Serengeti iliweka kambi nchini Rwanda kujiandaa na mechi hiyo ya mwisho ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa vijana wa umri huo.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, mkuu wa msafara wa kikosi hicho Ayoub Nyenzi alisema wachezaji wote wako salama tayari kwa mechi hiyo.

Mechi hiyo ni muhimu kwa timu zote mbili kwani itakayoshinda itafuzu fainali hizo zitakazofanyika Madagascar mwakani.

Serengeti Boys inaingia uwanjani ikiwa mbele kwa mabao 3-2 iliyoyapata katika mechi ya kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam takriban wiki mbili zilizopita.

Hivyo katika mechi hiyo inahitaji kulinda mabao yake huku ikijitahidi kuongeza mengine ili ijiweke salama katika kufuzu fainali hizo.

Endapo itafuzu itakuwa ni mara ya kwanza kwa timu ya vijana kufanya hivyo.

Mwaka 2005 Serengeti ilifuzu kwenye michuano iliyofanyika Gambia lakini ikaondolewa baada ya kubainika kuchezesha mchezaji aliyezidi umri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *