Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta leo anatarajiwa kuiongoza tena KRC Genk katika mchezo wa kwanza wa Kundi F Europa Ligi dhidi ya wenyeji, Rapid Viena nchini Austria.

SK Rapid Wien watakuwa wenyeji wa KRC Genk Uwanja wa Allianz, wakati katika mchezo mwingine wa kundi hilo, Sassuolo ya Italia watakuwa wenyeji wa Athletic Bilbao ya Hispania Uwanja wa Citta del Tricolore.

Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 24 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na sita msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.

Katika mechi hizo, ni 13 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na tatu msimu huu, wakati 11 alitokea benchi nane msimu uliopita na tatu msimu huu na mechi nane hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na mbili msimu huu.

Mchezo huu utakuwa wa pili tangu Samatta arejee Ulaya, akitokea kuichezea timu yake ya taifa, Taifa Stars ikipigwa 1-0 na Nigeria katika mchezo wa mwisho wa Kundi G kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *